KAZI KIMATAIFA BADO IPO

KUPATA ushindi kwenye mechi za hatua ya makundi na kutinga hatua ya robo fainali hakika hili ni kubwa kwa timu zote ambazo zimefanikisha jambo hilo.

Unaona kila mchezaji alikuwa anajituma kwenye mechi za nyumbani na ugenini katika kusaka ushindi na mwisho imekuwa hivyo.

Mashindano ambayo yanafuatiliwa na watu wengi yameleta matokeo mazuri kwa kila timu hili sio jambo jepesi kwani kupata matokeo katika mashindano ya kimataifa ni lazima upambane.

Kwa hatua ambazo Simba na Yanga zimefikia bado kazi ipo ni lazima ‘wagangangamale’ zaidi kupata matokeo mazuri kwenye hatua ya robo fainali ambayo wamefika.

Simba kwenye Ligi ya Maingwa Afrika na Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika kila mmoja ameshamtambua mpinzani wake na namna ubora ulivyo.

Kila hatua ni ngumu na kila timu ina mpinzani mkubwa na mgumu hivyo muhimu kwa sasa kuongeza umakini kwenye maandalizi pamoja na kuchukua tahadhari muhimu katika kutafuta matokeo wakati ujao.

Hakuna ambaye hajafanya jambo kubwa licha ya mwanzo kwa kila mmoja kuwa ulikuwa ni wa kusuasua katika mechi za mwanzo na mipango ilipokaa sawa ushindi ulikuwa kwenu.

Hakika kwa wale ambao walikuwa wanazifuatilia timu mwanzo tamaa ilikuwa ni kimbilio lao lakini kwenye ulimwengu wa mpira tunasema mpira unadunda na matokeo ni mpaka dakika 90 zikamilike.

Mwisho kila kitu sasa kipo wazi na mbichi na mbivu zimejulikana kwenye hatua ya makundi na sasa kwenye hatua ya robo fainali kazi itakuwa ngumu zaidi.

Ugumu wake ni kutokana na mechi kuwa mbili na mshindi wa jumla yeye ana kazi ya kutinga hatua ya nusu fainali hivyo kila mchezo ni zaidi ya fainali.

Kwa hatua ambayo mmefika ya robo fainali ni mchezo mmoja nyumbani na ugenini na hapa ni ushindi sio msako wa pointi hili nalo ni jambo la msingi kukaa akilini kwa wachezaji mapema.

Kazi haijaisha inaendelea hivyo vita yenu ilivyokuwa kwenye hatua za makundi basi iwe kwenye hatua ya robo fainali.

Mashabiki wenu wamefurahi, Tanzania pia imefurahi kwa kuwa kila mmoja sasa anazungumza wimbo mmoja ushindi kwenye anga za kimataifa.

Jambo la msingi kwenye hatua ya robo fainali ni kuendeleza ile furaha ambayo ilikuwa imekosekana kwa muda mrefu kwa wakati mmoja kwa timu hizi mbili.

Kila ushindi ni zawadi kwa Watanzania na inawezekana ikiwa mtaamua kufanya maadalizi mazuri kwa wakati huu uliopo.

Ipo wazi kuwa namna unavyozidi kuyafikia mafanikio na vikwazo vinazidi kuongezeka hivyo ni muhimu kulitambua hilo na kulifanyia kazi.

Hakuna ambaye atakuwa na kazi nyepesi kwenye hatua ya robo fainali na akipenya hapo kuna kigongo cha nusu fainali nacho hakikatakuwa chepesi.

Muhimu kwenye hizi mechi za hatua ya robo fainali kila mmoja kufanya vizuri na kupata ushindi nyumbani ana ugenini kisha baada ya hapo mipango ya nusu fainali inabidi ifuatwe.