>

CONTE KASEPA NA KAKA YAKE SPURS

KOCHA Antonio Conte ameripotiwa kutoa baraka zake kwa wakufunzi wake kusalia Tottenham Hotspur – lakini kaka yake Gianluca anatazamiwa kumfuata kwenye safari ya kuondoka klabuni hapo.

Muitaliano huyo hatimaye anaondoka Spurs kwa makubaliano ya pande zote kufuatia kutoa maneno ya kejeli dhidi ya wachezaji wake baada ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Southampton mapema mwezi huu licha ya kuongoza kwa mabao 3-1 hadi dk ya 76.

Msaidizi wa muda mrefu wa Conte, Cristian Stellini atakuwa kaimu kocha mkuu, huku Ryan Mason msaidizi kwa muda uliosalia wa msimu.

Gazeti la Evening Standard liliripoti kwamba, Stellini atabaki na baadhi ya wafanyakazi wa Conte, wakiwemo kocha wa makipa Marco Savorani, mtaalamu wa mazoezi ya viungo, Gianni Vio na wakufunzi wa mazoezi ya viungo, Stefano Bruno na Constantino Coratti.

Hata hivyo, ripoti hiyo inadai Gianluca Conte, ambaye alikuwa akifanya kazi kama kocha wa kiufundi na uchambuzi, atamfuata kaka yake nje ya klabu.

Savorani ndiye aliyekuwa na uwezekano mkubwa wa kuondoka na Conte lakini atabaki kumsaidia Stellini kwenye michezo 10 iliyobaki ya Premier League huku lengo lao likiwa ni kumaliza ndani ya top four.

Spurs wako nafasi ya nne lakini Newcastle walio katika nafasi ya tano wapo nyuma kwa pointi mbili tu na wana michezo miwili mkononi.

Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy na uongozi wa klabu wataanza msako mwingine wa kocha huku bosi aliyefukuzwa kazi hivi majuzi pale Bayern Munich, Julian Nagelsmann na kipenzi cha zamani cha Spurs, Mauricio Pochettino miongoni mwa majina yanayotajwa.