MSAKO WA VIPAJI UWE NA MWENDELEZO

MWENDELEZO mzuri kwenye uwekezaji kwa vijana unahitajika kuwa wa vitendo kwa kila timu na sio kuishia kupiga picha na porojo ambazo zinaishi kila siku.

Ipo wazi kwa sasa vijana wengi wanaopewa nafasi kikosi cha kwanza kwenye timu za wakubwa wanahesibaki hasa ukiziweka kando Azam FC, Mtibwa Sugar, Ihefu na Kagera Sugar.

Kuna timu ni ngumu kuwapa nafasi wachezaji kutoka timu za vijana jambo linalofanya wachezaji wengi kukosa nafasi ya kupanda na kuishia kwenye timu za vijana mpaka muda wao utakapogota mwisho.

Simba inajivunia kizazi kile cha Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, huku Jonas Mkude akiwa ni yeye pekee amebaki ndani ya kikosi cha Simba.

Kwa haya ambayo yanafanyika ni muhimu kwa wachezaji kuongeza juhudi ili wapewe nafasi kikosi cha kwanza pamoja na makocha kuwapa nafasi vijana waonyeshe uwezo wao.

Ukweli ni kwamba makocha wanapenda kuwatumia wachezaji vijana lakini pale wanapopewa nafasi wameonekana kucheza chini ya kiwango jambo linalowapa kazi kuwaamini wakati ujao.

Pia kumekuwa na mipango mingi kwenye maandishi pamoja na maneno kuhusu uwezo wa kuwainua vijana na kuwapa nafasi lakini mipango hiyo imekuwa inakwenda na maji.

Ili kuwa na timu imara kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ni muhimu kuwa na wachezaji wazuri kwenye vikosi vya timu kubwa na hili linawezekana ikiwa litakuwa endelevu.

Wachezaji mkipata nafasi kwenye timu kubwa hasa vijana ni muhimu kuonyesha kitu cha pekee ili mpate nafasi ya kudumu.

Mipango ya kuibua vipaji kwa vijana ni muhimu kupewa kipaumbele kwa vitendo na hili litafanya kuwe na ubora kwenye kila idara kutoka kwa wazawa.