RASHFORD, OSIMHEN, MBAPPE HAWAZUILIKI

SAPRAIZI za kutosha zilijiri wikiendi iliyopita ndani ya ligi tano bora Ulaya.

Hii ni kwa namna mambo yalivyoonekana katika viwanja  tofauti kwenye ligi za Bundesliga, La Liga, Serie A, Premier League na Ligue 1.

Huko Ulaya vita ilikuwa kali lakini kuna mastaa walionekana kuendelea kutisha kwa kuzibeba timu zao kama Marcus Rashford, Victor Osimhen, Kylian Mbappe na Federico Valverde.

Kwa ujumla ndani ya Ulaya wikiendi mambo yalikuwa hivi kama ambavyo makala haya yanakuchambulia.

MESSI, MBAPPE, NEYMAR WAWASHA MOTO

Ngoma ilikuwa ngumu kwa Paris Saint-Germain wakivaana na Lille nyumbani licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 kwa mabao ya Kylian Mbappe (2), Neymar na Lionel Messi. Ushindi huo umekuja baada ya timu hiyo kutoka kupoteza mechi tatu mfululizo za michuano yote.

LIVERPOOL IS BACK

Liverpool ambao walikuwa wamepotea ndani ya Premier League, kwa sasa ni kama wameamka baada ya wikiendi kuichapa Newcastle United mabao 2-0.

Huu ulikuwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa Liverpool ndani ya ligi tangu tuanze mwaka 2023, wakitoka kuifunga Everton. Kumbuka kipigo hicho ni cha pili kwa Newcastle United katika Premier na vyote hivyo wamepokea kutoka kwa Liverpool.

NAPOLI UNSTOPPABLE

Kazi wanayofanya huko Serie A siyo ya kitoto kutokana na aina ya matokeo ambayo wamekuwa wakipata. Safari hii waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sassuolo, matokeo hayo yameifanya Napoli kuwa kileleni kwa tofauti ya pointi 18. Kubwa zaidi katika mchezo huo Khvicha Kvaratskhelia  na Victor Osimhen walifunga.

ARSENAL HATARI

Baada ya kuyumba katika mechi tatu mfululizo za Premier, wikiendi Arsenal haikumuacha mtu salama licha ya kuwa ugenini ndani ya Dimba la Villa Park, baada ya kushinda mabao 2-4. Ushindi huo uliifanya timu hiyo kurudi kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 54.

BAYERN YAPEWA SAPRAIZI YA KIPIGO

Bayern Munich ikiwa ugenini, ilipoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya wenyeji wao Borussia Mönchengladbach. Kitendo cha Bayern kupoteza ni wazi mbio za ubingwa zinazidi kuwa ngumu.

CHELSEA YADUWAZWA NA KIBONDE

Mambo bado magumu kwa Chelsea baada ya kupoteza mbele ya Southampton kwa bao 1-0. Chelsea wameendelea kuwa katika wakati mgumu licha ya kufanya usajili wa bei mbaya.

VALVERDE HUKO MADRID HATARI

Federico Valverde wikiendi aliendelea kukomaa kuhakikisha Madrid inapata matokeo bora na kocha wake Carlo Ancelotti anasalia hapo. Madrid ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Osasuna  na kuipa timu hiyo pointi tatu.

MAN CITY YATIKISWA

Wakiwa ugenini, Manchester City kwao mambo yalikuwa magumu baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Nottingham Forest.

DORTMUND YAGAWA DOZI

Wakiwa nyumbani, Borussia Dortmund walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Hertha Berlin na kuifanya timu hiyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa wa Bundesliga ambao msimu huu ni kama hauna mwenyewe.

INTER WAICHAPA UDINESE

Mambo yalikuwa mazuri kwa Inter Milan ambao walikuwa wakicheza dhidi ya Udinese na kushinda 3-1.

FANTASTIC RASHFORD

Marcus Rashford alikuwa mwiba tena wakati Manchester United ikifanikiwa kuisambaratisha Leicester City kwa mabao 3-0. Katika mchezo huo, Rashford alifunga mabao mawili likiwa ni bao lake la 16 tangu kumalizika kwa Kombe la Dunia 2022 na kuifanya Man United kufikisha pointi 49 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo.

BARCELONA YAENDELEA KUKIMBIZA

Clean sheet ya 17 kwa Barcelona iliendelea baada ya kufanikiwa kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Cadiz. Barcelona ilitisha kwa kupata ushindi huo kwa mabao Robert Lewandowski akifunga bao lake la 15 baada ya kucheza mechi tano bila bao.

LONDON DABI ILIKUWA NOMA

Tottenham walikuwa noma ndani ya London Dabi mara baada ya kuisambaratisha West Ham United kwa mabao 2-0. Ushindi huo umeifanya Tottenham kutinga ndani ya nne bora kwa kuitoa Newcastle United.