NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa watabadili mbinu kwenye mchezo wao dhidi ya TP Mazembe huku akija kwa utofauti kulingana na mchezo husika.
Nabi alikuwa benchi kwenye mchezo uliopita ugenini wa hatua ya makundi aliposhuhudia ubao ukisoma US Monastir 2-0 Yanga nchini Tunisia.
Leo unatarajiwa kuchezwa mchezo wa pili dhidi ya TP Mazembe ambao wametoka kupata ushindi dhidi ya Real Bamako kwenye mchezo wao uliopita kwa mabao 3-1.
Nabi amesema kuwa kila mchezo una mbinu zake tofauti kulingana na aina ya wapinzani wao jambo linalowapa nguvu ya kuingia uwanjani kusaka ushindi.
“Ikiwa umepoteza mchezo wa kwanza haina maana kwamba inakuwa ni mwisho wa kuendelea kupambana, yale ambayo yamepita tunasahau na kuanza kufanya maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu unaofuata.
“Huwa sipendi sana kuzungumza unajua hasa ukizingatia mimi ni mtu wa mpira, ninapenda kuona wachezaji wakicheza na kupata ushindi kwa namna ambavyo wapinzani wetu watakuwa ndivyo ambavyo nasi tunapanga kikosi chetu.
“Mbinu ambazo zilitumika ugenini ama kwenye mchezo ambao tulipoteza hatuwezi kuzirudia kwa wakati mwingine, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” alisema Nabi.
Ni Bernard Morrison na Aboutwalib Mshery ambaye ni kipa hawa wanatarajiwa kuukosa mchezo wa leo kwa kuwa hawapo fiti.