YANGA MACHO YOTE KWA TP MAZEMBE

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa kwa sasa hesabu kubwa ni kwenye mchezo wao wa Jumapili dhidi ya TP Mazembe huku yale yaliyotokea Tunisia wakiyaweka kando.

Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi Februari 12 ilishuhudia ubao ukisoma US Monastir 2-0 Yanga kwenye mchezo wa hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Afrika.

Jana msafara wa Yanga uliwasili Dar ukitokea Guinea ambapo ulipitia Dubai ukiwa umeongozana na wachezaji wake pamoja na benchi la ufundi na miongoni mwa viongozi hao akiwa ni Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe.

Wachezaji ni pamoja na Disckon Job, Bakari Mwamnyeto, Fiston Mayele, Jesus Moloko, Aboutwalib Mshery .

Kamwe amesema kuwa haikuwa mpango wao kupoteza lakini imetokea kwa kuwa ni mpira na matokeo hayawezi kubadilika.

“Hatukuwa na mpango wakupoteza kwenye mchezo wetu lakini imetokea. Kwa yale ambayo yametokea tumeyasahu yote na akili zetu ni kwenye mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe.

“Huo ni mchezo muhimu kwetu kupata ushindi na ukizingatia kwamba tutakuwa nyumbani, wachezaji na benchi la ufundi wamekubaliana kufanya kazi kwelikweli na inawezekana hivyo mashabiki mjitokeze kwa wingi,” amesema Kamwe.