MTOKO wa kifamilia kwa Simba ikiwa ni mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Al Hilal wametoshana nguvu Uwanja wa Mkapa.
Baada ya dakika 90 ubao umesoma Simba 1-1 Al Hilal ambapo dakika 45 za mwanzo zilikuwa mali ya Al Hilal kisha Simba wakafanya kazi kubwa kipindi cha pili.
Bao la Al Hilal limefungwa kwa mpango mzuri wa pigo la faulo iliyojazwa kimiani na Makabi Lilepo dakika ya 7 ambalo lilimshinda mlinda mlango wa Simba Beno Kakolanya.
Shukrani kwa Habib Kyombo ambaye alionyesha utulivu mkubwa dakika ya 81 akiwa ndani ya 18 mzawa huyo alipachika bao la kuweka usawa.
Kyombo kwenye mchezo wa leo alianzia benchi alichukua nafasi ya Okra ambaye alipata maumivu ilikuwa dakika ya 15.
Ni pasi ya nyota Pape Sakho ambaye uwezo wake huwa ni maji kupwa kujaa alimwaga majalo yalitokutana na Kyombo.
Mchezo huo ni maandalizi kwa ajili ya mechi za kimataifa ambapo timu zote zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.