KAMA Morocco ingepata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2010, Uwanja wa Adrar ulipangwa kutumika kwenye moja ya michezo muhimu ya mtoano ya hatua ya robo fainali.
Bahati mbaya kwa Morocco, nafasi hiyo ikaenda kwa Afrika Kusini na baada ya hapo, wakaamua kuendeleza taratibu ujenzi wa uwanja huo hadi ulipokamilika na mwaka 2013 ukawa sehemu ya viwanja vilivyochezewa Kombe la Dunia la klabu.
Morocco ndiyo nchi pekee ya Afrika imewahi kuandaa fainali za Kombe la Dunia la klabu, tena mara mbili na Uwanja wa Adrar tayari una sifa ya kuwa viwanja vichache vya Afrika vilivyo na bora zaidi.
Uwanja huo una uwezo wa kuingiza watazamaji 45,480 na ninaweza kusema kama utautazama kwa nje, si uwanja wenye mvuto sana tofauti na ukiingia ndani.
Nje una mfumo wa muonekano kama ngazi hivi au majukwaa ambayo hayana viti na wahusika wakati tulipotembelea katika uwanja huo juzi, wanasema waliamua kufanya ubunifu huo ili uwanja huo uendane na mazingira.
Mji wa Agadir uko tofauti na miji mingine ya Morocco, licha ya kwamba kuna kilimo kikubwa cha umwagiliaji Jirani na milima ya Atlas, lakini ni mji mkavu ambao unaonyesha jangwa.
Tofauto na Rabat au Casablanca unaweza kuona sehemu nyingi za kijani kwa asilia kabisa. Agadir kidogo kuna tofauti na ni mji uliotulia sana.
Ndani ya uwanja huo ni tofauti sana na viwanja vingi ambavyo nimewahi kuingia. Haswa suala la kuwa na sehemu maalum ya wachezaji kupasha misuli ndani kwa ndani badala ya kutoka nje.
Sehemu hiyo inawapa nafasi wachezaji kupasha kabla ya kuingia uwanjani, maana yake wanapokwenda uwanjani wanakuwa tayari kabisa kwa mchezo.
Eneo hilo ni kubwa na liko kwa ndani ya uwanja karibu na vyumba vya kubadilishia nguo. Hii ni nadra kuona kwa viwanja vingi sana.
Achana na hivyo, vyumba vinne vya kubadilishia nguo, vyumba viwili vya waamuzi ni vya kisasa kabisa kutokana na kuwa na muundo wa kuvutia sana.
Ndani ya vyumba hivyo kuna sehemu maalum ya jacus, maji ya moto na vyoo vilivyotengenezwa mfano wa nyumba za matajiri, hali inayowafanya wachezaji kujisikia wako katika eneo tulivu wakati wakijiandaa na mchezo baada ya kuingia uwanjani.
Hassania Agadir ndio timu inayoutumia uwanja huo kama uwanja wa nyumbani, mashabiki wake wamekuwa na uhakika kutokana na mifumo bora ya usalama kuanzia kamera za kutosha lakini umetengenezwa kisasa zaidi na kuwafanya walinzi kuwa na nafasi nzuri kujipanga kiusalama kwa ajili ya mashabiki watukutu.
Ndani ya uwanja huo kuna vyumba viwili vikubwa kwa ajili ya matibabu na gari la wagonjwa hukaa tayari kama kuna tatizo la dharura kwa mchezaji, mashabiki au wadau wengine.
Naweza kusema ni moja ya viwanja bora nimewahi kuhudhuria na kuona ubora wake na ndio maana Morocco wameamua kukiweka kati ya viwanja vyake bora katika kuwania kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia.
Mwaka 2026, moja ya nchi za Afrika zitakazowania nafasi hiyo ya kuandaa Kombe la Dunia ni Morocco ambayo inaonekana imejipanga hasa.
Adrar ambao ni uwanja wa nyasi asilia, ni sehemu ya kuonesha Morocco wako tayari na licha ya kwamba ulianza kutumika mwaka 2013, ukiingia unaweza kufikiri ni kati ya viwanja vilivyojengwa miezi mitano au sita iliyopita.
Uwanja huo, una nafasi kubwa kwa nje kwa maana ya maegesho makubwa ya magari lakini mageti 16 ambayo yanatoa nafasi kwa watu kuingia na kutoka kwa wepesi mara tu baada ya mechi.
Adrar ni hazina ya Morocco lakini ni hazina ya Afrika kwa maana ya maendeleo ya mchezo wa soka na kama nchi nyingi za Afrika zitaendelea kujiimarisha kama Morocco, kuwa na viwanja mfano wa Adrar, bila shaka Afrika itaendelea kupiga hatua kubwa katika mchezo wa soka na kuendelea kuisumbua dunia.