ASANTE JANUARI, KARIBU MWEZI WA UPENDO

YAPO mengimengi ambayo yanakatisha tamaa lakini yasikupe maumivu ukaacha kupambana kwa ajili ya kufikia malengo.

Ilikua hivyo Januari Mosi kwenye mapambano na sasa ni Januari 31, unadhani unaweza kusema nini zaidi ya asante Januari, karibu mwezi wa upendo Februari.

Yote kwa yote kuna matukio ambayo yalitokea ndani ya Januari yataishi kwenye kumbukumbu namna hii katika ulimwengu wa mpira:-

Zawadi ya Ruvu Shooting

Wakiwa kwenye mwendo ambao hauwafurahishi, Ruvu Shooting waliweka wazi kuwa wamewapa zawadi ya ushindi Yanga kwa kuwa bao lililowapa pointi tatu mchezaji wao Mpoki Mwakinyuke alijifunga dakika ya 33.

Kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 1-0 Ruvu Shooting na kuipa pointi tatu mazima Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.

Mlandege wametisha

Mlandege ya visiwani Zanzibar walitisha kwa kuwakalisha chini vigogo wote waliokuwa wanawania taji la Mapinduzi 2023.

Kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Singida Big Stars waliwatungua mabao 2-1 na kutwaa taji hilo ambalo lilikuwa na ushindani mkubwa.

Ikumbukwe kwamba Mlandege hao waliwatungua mabingwa watetezi Simba kwenye mchezo wa makundi kwa kuwafunga bao 1-0 ambalo liliwaondoa kwenye reli jumlajumla.

Mwendo wa 7/7

Watani wa jadi beto lao huwa haliishi na ukimkopesha mwenzako lazima akulipe kwa mtindo ambao anautambua yeye hata muda upite namna gani.

Unakumbuka wakati tukifunga majalada ya 2022, ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 7-1 Tanzania Prisons? Ilikuwa ni Desemba 30.

Kwenye funga Januari, Yanga wakaibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Rhino Rangers, lakini ilikuwa ni kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho na Yanga inatinga hatua ya 16 bora wakiwa ni mabingwa watetezi.

Sey kama Sey

Mwamba huyu hapa Stephen Sey karejea ndani ya Dodoma Jiji, kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam FC hakuwa na bahati kwa kuwa alikosa penalti baada ya kuipaisha.

Ilikuwa ni Januari 27 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Azam FC 4-1 Dodoma Jiji, Sey alikosa penalti hiyo dakika ya 44 ikiwa ni mchezo wake wa kwanza kucheza baada ya kujiunga na timu hiyo inayonolewa na Melis Medo.

Mwingine ambaye alifunga Januari kwa mtindo huo pia ni Clement Mzize nyota wa Yanga mwenye mabao manne kwenye Kombe la Shirikisho ambapo alikwama kumtungua Mohamed Ally kwa mkwaju wa penalti dakika ya 82 baada ya kipa huyo kuipangua.

Chama na Mbarazil wake

Clatous Chama nyota wa Simba Januari 18 ilikuwa ni siku mbaya kazini baada ya Kocha Mkuu,Roerto Oliviera kumfanyia mabadiliko dakika ya 33, jambo ambalo lilizua gumzo.

Wakati Chama anatolewa alikuwa ametoa pasi yake ya 12 kwa Saidi Ntibanzokiza na ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 3-2 Mbeya City na nafasi ya Chama ilichukuliwa na Pape Sakho.

Chama hakuwa kwenye mchezo wa pili dhidi ya Dodoma Jiji kwa kile kilichoelezwa kuwa anasumbuliwa na Malaria.

Uchaguzi wa Simba

Ngoma ilikuwa nzito kwenye suala la uchaguzi mkuu wa Simba ambapo Januari 29,2023 uchaguzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Julisu Nyerere.

Mpaka saa tatu usiku ngoma ilikuwa ni bilabila hakuna majibu ya nani kashinda jambo ambalo liliibua mijadala.

Mwisho ni Murtanza Mangungu alitangazwa kuwa mshindi kwenye nafasi ya uenyekiti akitetea kiti chake na wajumbe ikiwa ni pamoja na Asha Baraka.

Makala hii imeandikwa na Dizo Click na ipo kwenye gazeti la Spoti Xtra Jumanne, Januari 31,2023.