FEI TOTO AMPASUA KICHWA NABI YANGA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameibuka na kuvunja ukimya kwa kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu akiwemo kiungo Feisal Salumu ‘Fei Toto’ kumesababisha kumpa wakati mgumu wa kupata matokeo katika michezo yao.

Nabi ametoa kauli hiyo kufuatia Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo uliopigwa juzi Jumatatu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Yanga imewakosa viungo wake, Khalid Aucho ambaye amepata majereha na Fei Totot aliye kwenye mgogoro na uongozi wa timu hiyo.

Akizungumza na Championi Jumatano, Nabi alisema kuwa, kukosekana kwa wachezaji hao kumesababisha kupata matokeo ya kusuasusa licha ya kupata muda wa kutosha wa kujiandaa na mchezo huo ambao walistahili kupata matokeo makubwa.

“Kwetu haikuwa nzuri sana kutokana na maandalizi ambayo tumefanya kwa siku saba kabla ya mchezo wenyewe kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji wetu muhimu, hakuwepo Aucho, Morison pamoja na Feisal kitu ambacho kimechangia kupata matokeo ya aina hii.

“Lakini tunachokiangalia kwa sasa ni kuweza kurekebisha hali hii kwa kuhakikisha tunakuwa bora katika michezo iliokuwa mbele yetu kwa sababu naamini watakuwa wamerudi maana hata mfumo ambao tulikuwa tunaujaribu hakuweza kutupa kile ambacho tulikuwa tunahitaji,” alisema Nabi.