NYOTA HUYU ALIKUWA SABABU KWA MABAO KWA TIMU ZOTE MBILI

MCHEZO wa mpira ni mchezo wa makosa na wanasema ukifanya kosa moja unaadhabiwa na mpinzani wako.

Miongoni mwa mchezo ambao ulikuwa unasubiriwa kwa shauku kubwa ni ule wa fungua mwaka kwa Simba iliyoweka kambi Dubai kwa muda.

Pia ilikuwa na kocha mpya kwenye benchi ambaye ni Robert Oliviera hakika mashabiki walikuwa wanasubiri kuona namna kazi itakavyokuwa dhidi ya Mbeya City.

Kwenye mchezo huo Mbeya City walikamilisha dakika 90 wakiwa pungufu baada ya nyota wao Samson Madeleke kuonyeshwa kadi mbili za njano jambo lililofanya akaonyeshwa kadi nyekunduna ubao ulisoma Simba 3-2 Mbeya City.

Ni Mohamed Hussein Zimbwe Jr, dakika ya 45 alichezewa faulo ndani ya 18 eneo la Mbeya City mwamuzi akaamuru lipigwe tuta licha ya wachezaji wa Mbeya City kuonekana kuigomea.

Mtupiaji alikuwa ni Saidi Ntibanzokiza dakika ya 48 na Hassan Nassoro alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Mbeya City walioonyeshwa kadi ya njano kutokana na faulo hiyo.

Huyohuyo Zimbwe kama ambavyo wanasema ukiua kwa upanga nawe utauliwa kwa upanga alicheza faulo dakika ya 77 wachezaji wa Simba wakiwa hawajajipanga ilipigwa faulo ya harakaharaka na Juma Shemvuni.

Kilichomkuta Aishi Manula dakika ya 78 haamini macho yake ngoma ilizama mazima nyavuni kwenye mchezo huo ambao ubao ulikamilika Simba 3-2 Mbeya City.

Ikumbukwe kwamba sio mchezaji wa kwanza kufanya makosa kwenye mpira wa soka kuna wakati nyota Abal Kassim wakati huo akiwa ndani ya Kagera Sugar alijifunga bao mbele ya Yanga kisha akawafunga pia wapinzani wao Yanga.