KARIBU kwenye mapigo ya ligi ambayo yanaendelea ikiwa ni mwaka 2023, Uwanja wa Mkapa utakuwa na kazi ndani ya dakika 90 kwa wababe kusaka pointi tatu.
Ni Yanga dhidi ya Ihefu mchezo unaosubiriwa kwa shauku kubwa kutokana na Ihefu kuwa watibuaji wa mipango ya Yanga.
Hapa tunakuletea baadhi ya mambo yatakayonogesha mchezo huo namna hii:-
Rekodi za 2023
Kwa Yanga ni mchezo wa kwanza kwao kwenye ligi 2023 baada ya kufunga 2022 Desemba 31,2022 ubao wa Uwanja wa Manungu ulisoma Mtibwa Sugar 0-1 Yanga.
Bao la ushindi lilifungwa na kiungo Aziz KI kwa pigo la faulo na anafikisha mabao manne ndani ya ligi.
Vinara hao wa ligi Yanga wanasaka rekodi kwenye mchezo huo ikiwa ni mchezo wao wa kwanza ndani ya 2023.
Januari 3,2023 walipata ushindi dhidi ya KMC ambapo ubao wa Uwanja wa Highland Estate ulisoma Ihefu 1-0 KMC.
Beki Ismail Gambo hakuwa na chaguo la kufanya kwenye harakati za kuokoa krosi iliyopigwa na Obrey Chirwa alijifunga na kuipa pointi tatu Ihefu inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mwambusi.
Ihefu wao wanasaka mwendelezo wa rekodi yao ndani ya 2023.
Kisasi
Ile kasi ya Yanga kutofungwa ndani ya ligi iligotea mbele ya Ihefu baada ya ubao wa Uwanja wa Highland Estate kusoma Ihefu 2-1 Yanga.
Mchezo huo ulichezwa Novemba 29 2022 na Yanga ilikuwa inasaka rekodi ya kufikisha mechi 50 bila kufungwa ngoma ikawa nzito.
Wanakutana uwanjani kwenye msako wa ushindi ambapo Yanga wanahitaji kulipa kisasi cha kutunguliwa ugenini na Ihefu wanahitaji ushindi.
Ukuta ngoma nzito
Yanga wanajivunia uwepo wa Yannick Bangala ambaye ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi akiwa ni mmoja ya wale aliowatungua Ihefu lakini leo hatakuwa kwenye kikosi cha kwanza.
Kwenye mabao mawili aliyonayo kibindoni moja kawatungua Ihefu na bao moja aliwatungua Namungo licha ya kuwa ni beki na timu hiyo imeruhusu mabao 10 baada ya kucheza mechi 19.
Juma Nyosso anaunda ukuta wa Ihefu akiwa ni chaguo la kwanza la Mwambusi ukuta wa Ihefu umeokota mabao 22 kwenye mechi 19.
Mipira iliyokufa
Timu zote zina wataalamu wa mipira iliyokufa na hata mechi iliyopita chanzo cha mabao hayo ilikuwa ni mipira iliyokufa.
Ni Joyce Lomalisa alipiga pigo la faulo dakika ya 8 likakutana na kichwa cha Bangala na Ihefu wao ni Nivere Tigere aliyepiga pigo la faulo dakika ya 38 likazama mazima ndani ya nyavu za Djigui Diarra.
Hata bao la ushindi lililofungwa na Lenny Kissu mpango kazi ulitengenezwa na Tigere aliyepiga kona iliyoleta bao la ushindi kwenye mchezo huo.
Vyuma vipya
Timu zote mbili zina maingizo mapya ambapo kwa Yanga wamemtambulisha Mudathir Yahaya ambaye ni kiungo huku Ihefu wao wakiwa wamemtambulisha Adam Adam yeye ni mshambuliaji.
Ikiwa watapata nafasi za kuanza nyota hawa watakuwa na kazi ya kuonyesha uwezo wao kwenye timu zao mpya.
Ofisa Habari wa Yanga,Ali Kamwe amesema kuwa wanatambua walipoteza mchezo wa kwanza walipokutana wamejipanga kupata ushindi.
“Tulipoteza kwenye mchezo wa kwanza tulipokutana nao na sasa tunakwenda kukutana nao kwenye mchezo wa pili tunahitaji kupata matokeo na tupo tayari,”.
Peter Andrew, Ofisa Habari wa Ihefu FC amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mechi zao zote.
“Tupo tayari kwa ajili ya mechi zetu zote kupata matokeo na tunaamini kwamba kazi itafanyika,”.