YANGA YAMTEMBELEA MAMA KARUME

UONGOZI wa Yanga chini ya rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, benchi la ufundi, wachezaji pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, mapema jana Jumamosi walimtembelea mama Fatuma Karume ambaye ni mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na kumpa zawadi mbalimbali ikiwemo jezi za timu hiyo.

Hafla hiyo imefanyika nyumbani kwa mama Fatuma, Maisara mjini Unguja ambapo pia Yanga walimkabidhi makombe waliyoshinda msimu uliopita na msimu huu ya Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii mbili na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Mama Fatuma aliwashukuru Yanga kwa kumtembelea na kumpa zawadi hizo, huku akikubali ombi la kuwa mjumbe wa kudumu klabuni hapo.

Mbali na hayo, mama Fatuma aliwataka wachezaji kuwa wamoja, kuheshimu wakubwa na wadogo na pia nguvu zao kuelekeza katika kufikia malengo.

Yanga ambayo ilikuwa visiwani hapa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, iliondoka jana baada ya kutolewa hatua ya makundi.