AZAM FC WANALITAKA KOMBE LA SIMBA

UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa unalitaka Kombe la Mapinduzi hivyo hawatafanya makosa kwenye mashindano hayo.

Ni Simba ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo la heshima ambalo limeanza Januari 2023, visiwani Zanzibar.

 Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe amesema kuwa wanatambua ushindani ni mkubwa lakini wamedhamiria kufanya kweli.

“Hatuna utani raundi hii tunahitaji kutwaa makombe na kwenye Mapinduzi Cup tuna amini kwamba tutafanya vizuri hasa ukizingatia kwamba wachezaji wapo vizuri.

“Tuna kikosi cha kushindana na wapinzani wetu huku tukitanguliza heshima kwa wapinzani wetu kwani mpira ni mchezo wa makosa na mbinu, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” amesema Ibwe.

Msafara mzima wa kikosi cha Azam FC chini ya Kali Ongala uliibuka ndani ya Zanzibar Januari 2,2023.

Miongoni mwa wachezaji ambao wapo na kikosi hicho ni pamoja na Abdul Suleiman, ‘Sopu’ Prince Dube, Ayoub Lyanga.

Azam FC ipo kundi A ikiwa pamoja na Malindi na Jamhuri ambapo kwenye mchezo waliocheza Januari Mosi Malindi ilishinda mabao 2-0.

Azam FC mchezo wao unatarajiwa kuwa leo Januari 3,2023 dhidi ya Malindi saa 10:15 jioni.