AZAM FC V YANGA VITA YA DAKIKA 90

CEDRICK Kaze, kocha msaidizi wa Yanga amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Azam FC utakuwa mgumu lakini wamefanyia kazi makosa waliyofanya kwenye mzunguko wa kwanza hasa katika mipira ya adhabu.

Dakika 90 zitatoa majibu kwenye mchezo wa leo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu hizo mbli.

Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Yanga 2-2 Azam na kuwapa pointi mojamoja wababe hao.

Kaze amebainisha kuwa Azam FC ni moja ya timu yenye wachezaji wazuri lakini nao wamejiandaa kwa umakini ili kupata matokeo kwenye mchezo huo.

“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC kila mmoja atafanya kazi yake ili kupata matokeo na tunakumbuka mchezo uliopita tulipata pointi moja huku Azam FC wao mabao yao wakifunga kutokana na matumizi ya set pieces.

“Kwa makosa ambayo tulifanya kwenye mchezo wetu uliopita na mechi zetu ambazo tumecheza tumefanyia kazi na tuna amini kwamba tutapata matokeo mazuri,tunahitaji kuongeza pointi ili kuzidi kuwa karibu na kutwaa ubingwa,” amesema Kaze.

Kwa upande wa beki wa Yanga, Dickson Job alisema kuwa wachezaji watatoa zawadi ya Christmas kwa mashabiki wao.

“Zawadi tutakayotoa kwa mashabiki ni ushindi na tumekuwa tukipata matokeo kwenye mechi zetu kutokana na ushirikiano pamoja na mbinu ambazo tunapewa na benchi la ufundi,”.

John Matambala, kocha msaidizi wa Azam FC amesema kuwa wanatambua mchezo utakuwa mgumu na kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

“Tunatambua kwamba ushindani utakuwa mkubwa lakini ukweli ni kwamba tunawaheshimu wapinzani wetu na tunaamini utakuwa mchezo mzuri,” amesema.

Lusajo Mwaikenda nyota wa Azam FC amesema kuwa wana wachezaji wazuri na imara kwenye safu ya ushambuliaji jambo litakalowapa matokeo.

“Ushindani ni mkubwa na kila mmoja anatambua uhitaji wa pointi tatu muhimu kwenye mchezo wetu, wachezaji tupo tayari na tunawashambulaji wazuri,” amesema.

ReplyForward