>

SANTOS AICHA URENO YA CRISTIANO RONALDO

BAADA ya kuiongoza timu ya Taifa ya Ureno kwenye Kombe la Dunia 2022 Qatar na kutolewa katika hatua ya robo fainali na Timu ya Taifa ya Morocco, Fernando Santos aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo amesepa.

Baada ya kocha huyo kubwaga manyanga jina la kocha wa Roma, Jose Mourinho ni miongoni mwa jina linalotajwa kwa waliopendekezwa mapema kuchukua nafasi ya Santos.

Ikumbukwe kwamba kwenye mechi zake za mwisho Fernando Santos alichukua uamuzi mgumu kumuweka benchi Cristiano Ronaldo kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.

Kwenye mchezo wao dhidi ya Uswisi hatua ya 16 bora alianza na Goncalo Ramos kikosi cha kwanza badala ya Ronaldo ambapo mbadala wake huyo alifunga hat-trick katika ushindi wa 6-1 dhidi ya Uswizi.

Ronaldo aliingia kama mchezaji wa akiba katika mechi ya robo fainali dhidi ya Morocco lakini hakuweza kuipa ushindi timu hiyo kwenye mchezo huo.

Santos mara kwa mara alikabiliwa na maswali kuhusu kumwacha Ronaldo, huku mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United akikana ripoti iliyodai kuwa alitishia kuondoka Qatar kwa kutokuwa na mawasiliano mazuri na kocha wake.

 Mara kwa mara Santos alisisitiza kuwa hakuwa na majuto juu ya maamuzi juu ya Ronaldo, ambaye aliwaaga mashabaki wake akitokwa na machozi baada ya filimbi ya mwisho ya kichapo cha Morocco.

 Santos aliiongoza Ureno kushinda Euro 2016 na vile vile Ligi ya Mataifa ya 2018-19

 Shirikisho la Soka la Ureno lilisema ni “Wakati mwafaka wa kuanza mzunguko mpya” licha ya Santos kuwa chini ya mkataba hadi baada ya Euro 2024.

Ureno sasa wataanza mchakato wa kumteua kocha mkuu mpya, huku kocha wa Roma Jose Mourinho akiwa mmoja wa watu wanaopewa nafasi hiyo mapema.

Taarifa ya Shirikisho la Soka la Ureno ilisema: “Ilikuwa heshima kuwa na kocha na mtu kama Fernando Santos kwenye timu ya taifa.

 “FPF inamshukuru Fernando Santos na timu yake ya ufundi kwa muda wa miaka minane ya kipekee na inaamini kuwa shukrani hizi pia zinatolewa kwa niaba ya watu wa Ureno.

“Bodi ya FPF sasa itaanza mchakato wa kuchagua kocha wa kitaifa ajaye.”