>

MORROCO YAWEKA REKODI, URENO KAZI IMEISHA

MOROCCO inakuwa timu ya kwanza kutoka bara la Afrika kukata tiketi ya kufuzu hatua ya nusu Fainali kwenye Kombe la Dunia baada ya kupata ushindi mbele ya Timu ya Taifa ya Ureno.

Ni ushindi wa bao 1-0 ambao walipata kwenye mchezo huko kupitia kwa mshambuliaji wao Youssef En-Nesyri kwa pigo la kichwa dakika ya 42 amalo lilitosha kuipa tiketi timu hiyo kutinga hata ya nusu fainali Qatar 2022.

Dunia imepata mshituko kwenye ulimwengu wa michezo kwa kuwa hakuna ambaye alikuwa anaipa nafasi timu hiyo kupenya mbele ya Timu ya Taifa ya Ureno yenye Cristiano Ronaldo.

Juhudi za wachezaji wa Ureno kwenye mchezo huo ziligota mwamba kutokana na umakini wa wachezaji hao katika kulinda bao hilo ndani ya uwanja.

Ni Bruno Ferandes, Pepe, Joao Felix na CR 7 mwenyewe hawa walikuwa wakijaribu kuvunja ngome ya Morocco lakini walikwama kupata bao kwenye mchezo huo.

Ni wachezaji pungufu walimaliza kwenye mchezo huo baada ya nyota wao Walid Chedddira kuonyeshwa kadi mbili za njano dakika ya 90+3 iliyoambatana na kadi nyekundu.

Nahodha Ronaldo aliondoka uwanjani huku akilia huku akiaga kwani ndiyo michuano yake ya mwisho ya Kombe la Dunia kutokana na umri kumtupa mkono.

Ikumbukwe kwamba kabla ya mchezo huo Ureno ilikuwa imekutana na Morocco mara mbili kwenye michuano hiyo, Morocco ikishinda 3-1 hatua ya makundi 1986 Mexico na Ureno ikalipa kisasi kwa ushindi wa bao 1-0 nchini Urusi na  ushindi huo unakuwa ni wa pili kwa Morocco.

Timu hiyo sasa itakutana na mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Ufaransa ambao walitinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 England.