WAKULIMA kutoka Mbeya, Ihefu FC wamevunja mwiko wa Yanga kuendelea kucheza mechi za ligi bila kufungwa baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1.
Wakiwa Uwanja wa Highland Estate, Ihefu walianza kutunguliwa bao kipindi cha kwanza kupitia kwa kiraka Yanick Bangala dakika ya 8.
Ni Nivere Tigere aliweka usawa dakika ya 38 na kuwafanya waende mapumziko ngoma ikiwa imekaa sawa kwa timu zote kutoshana nguvu.
Kipindi cha pili Ihefu na Yanga walikuwa kwenye mtafutano na bao la ushindi likapachikwa na Lenny Kisu dakika ya 61 akiwa ndani ya 18.
Kisu alitumia makosa ya mabeki wa Yanga kutokuwa makini kwenye pigo la kona lililopigwa na Tigere na kuvunja mwendelezo wa timu hiyo kufikisha mechi 50 bila kufungwa.
Ikumbukwe kwamba Yanga imeweka rekodi ya kucheza mechi 49 za ligi bila kufungwa na timu ya mwisho kuifunga ilikuwa ni Azam FC.
Licha ya Yanga kupoteza bado ipo nafasi ya kwanza na pointi 32 kibindoni huku Ihefu ikiwa nafasi ya 13 ikipanda kutoka nafasi ya 16 baada ya kufikisha 11 kibindoni.