GHANA imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Korea Kusini kwenye mchezo wa Kombe la Dunia ambao unatajwa kuwa mmoja ya mchezo bora kutokea mwaka huu 2022 Qatar.
Nyota wa Ghana mwenye miaka 22 na siku 118 , Mohammed Kudus anakuwa staa wa pili kutoka Afrika mwenye umri mdogo kufunga mabao mawili kwenye Kombe la Dunia.
Wa kwanza alikuwa ni Ahmed Musa mwenye miaka 21
na siku 254 wa Nigeria alifunga Argentina mwaka 2014 wakati timu hiyo ilipopoteza kwa kufungwa mabao 3-2.
Kwenye mchezo wa kundi H mabao ya Ghana mawili yalifungwa na Kudus ilikuwa dakika ya 34 na 68 na lile moja ni mali ya Mohammed Salisu dakika ya 24.
Kwa upande wa Korea Kusini mabao yote yamepachikwa kimiani na Cho Gue-song dakika ya 58 na 61.
Mpaka dakika 90 zinagota mwisho ulipigwa msako wa maana kwa Korea Kusini ambao walikuwa wakisaka pointi moja na ngoma ikawa ngumu kwao kupenya.
Dakika za mwisho baada ya mwamuzi kumaliza mpira, Kocha Mkuu wa Korea Kusini Paulo Bento alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja labda ni kutokana na kuonekana akimlalamikia mwamuzi kwa kushindwa kuruhusu kona ya mwisho kupigwa kwa kuwa dakika za nyongeza zilikuwa zimeisha.