KIKOSI cha Singida Big Stars leo kina kazi ya kusaka pointi tatu muhimu mbele ya KMC ambao nao wanazihitaji pia.
Ni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Liti saa 8:00 mchana huko Singida.
Upande wa kiingilio ni 3,000 kwa mzunguko na VIP ni shilingi 5,000 ambazo zitawafanya mashabiki kushuhudia mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ikumbukwe kwamba Singida Big Stars wanashuka uwanjani baada ya mchezo wao uliopita ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Yanga 4-1 Singida Big Stars huku ubao wa Uwanja wa Uhuru ukisoma KMC 1-2 Dodoma jiji kwenye mechi yao iliyopita.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Singida Big Stars, Hussein Massanza amesema kuwa wamerejea Singida kwa ajili ya kusaka pointi tatu ambazo wanaamini watazifanyia kazi kubwa kuzitafuta.
“Kila kitu kinakwenda sawa na tunatambua kwamba wapinzani wetu KMC ni timu imara ambayo haitabiriki ambacho tunahitaji ni kupata ushindi mashabiki wawe pamoja nasi,”.