AWADH Juma, kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar amesema kuwa hasira zote za kupoteza kwenye mchezo wao dhidi ya Azam FC wanazipeleka kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union.
Mtibwa Sugar ilipoteza kwa kufungwa mabao 4-3 dhidi ya Azam FC mchezo uliochezwa Uwanja wa Manungu wikiendi iliyopita.
Leo Mtibwa Sugar ina kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Coastal Union ambayo imetoka kupata sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Mbeya City.
Juma amesema kuwa kila kitu kinakwenda sawa na baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Azam FC wanaelekeza nguvu kuikabili Coastal Union.
“Tumetoka kupoteza mchezo wetu dhidi ya Azam FC hilo lipo wazi na tunakwenda kuwakabili Coastal Union ambayo ni timu nzuri tunajua utakuwa mchezo mgumu lakini tunahitaji pointi tatu muhimu,” amesema.
Mtibwa Sugar ina pointi 15 baada ya kucheza mechi 11 inakutana na Coastal Union yenye pointi 12 baada ya mechi 9.
Coastal Union wameweka wazi kuwa wanahitaji pointi tatu mbele ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa leo.