SERENGETI GIRLS WAMETIMIZA MALENGO KOMBE LA DUNIA

BAKARI Shime, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17, Serengeti Girls amesema baada ya kufuzu robo fainali ya Kombe la Dunia Wanawake U 17, wametimiza malengo.

Serengeti Girls imefuzu hatua hiyo baada ya kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Canada na mtupiaji wa Tanzania ni Veronica Mapunda dakika ya 35.

Ni mara ya kwanza kwa Serengeti Girls kushiriki michuano hiyo inayofanyika India na imemaliza nafasi ya pili kwenye kundi D.

Shime amesema:”Kwenye mchezo wetu ambao ulitupa nafasi ya kufuzu robo fainali ilikuwa ni kazi kubwa kwa wachezaji kwa kuwa tulikuwa nyuma kwa bao moja lakini tulipambana kupata bao.

“Pongezi kwa wachezaji wangu kwa kujituma na kuonesha juhudi kubwa uwanjani mpaka kufanikiwa kufuzu robo fainali na ushindi huu ni kwa ajili ya Watanzania na tumefanikiwa kufikia malengo yetu,” amesema.

Mchezo ujao wa Serengeti ni dhidi ya Colombia ambao unatarajiwa kuchezwa kesho Oktoba 22 ambao utakuwa ni wa hatua ya robo fainali.