KOCHA Mkuu wa Simba, Juma Mgunda ametamba kuwa katika maisha yake ya soka hajawahi kuiogopa timu yoyote huku akitamba kuwa yupo tayari kwa ajili ya mapambano Kariakoo Dabi.
Kariakoo Dabi hiyo inatarajiwa kupigwa Jumapili saa kumi na moja kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Mgunda ataingia uwanjani akiwa na rekodi ya kufungwa na Yanga kwa njia ya penalti katika mchezo wa Fainali ya Kombe la FA ambao kwa dakika kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 zama hizo akiwa ndani ya Coastal Union ya Tanga.
Mgunda amesema kuwa maandalizi yamekamilika kwa asilimia mia moja na kikosi chake kipo fiti na tayari kupata matokeo ya mazuri ya ushindi.
Mgunda amesema kuwa anawaheshimu wapinzani wake Yanga, lakini sio kuwaogopa kwani wote wanatumia dakika 90 na miguu miwili ndani ya uwanja, hivyo hana hofu yoyote.
Aliongeza kuwa anajivunia ubora wa kikosi chake kinachoundwa na wachezaji wengi wenye ubora watakaoamua matokeo ndani ya dakika 90 akiwemo mshambuliaji wake tegemeo Moses Phiri.
“Nikiwa ni kocha kwangu, katika maisha yangju sijawahi kuiogopa timu yoyote zaidi ninaheshimu wapinzani yangu pekee.
“Tunakwenda kucheza dhidi ya Yanga, kwangu hii ni mara ya kwanza kuwepo katika benchi kwenye dabi hii kubwa ndani na nje ya nchi, kwani wengi wanaisubiria hiyo mechi.
“Niwaambie Yanga kwa, kikosi changu kipo fiti na tayari kupambana nao na kupata matokeo mazuri yatakayotubamkisha kukaa kileleni,” amesema Mgunda.