NYOTA wa kimataifa Karim Benzema ameshinda tuzo ya Ballon d’Or kwa upande wa wanaume kwa mara ya kwanza baada ya msimu mzuri akiwa na timu ya Real Madrid.
Timu hiyo imeweza kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kushinda mbele ya Liverpool na ilitwaa taji la Ligi Kuu ya Hispania maarufu kama La Liga.
Benzema, mwenye umri wa miaka 34, alikuwa na msimu wake bora zaidi kuwahi kutokea Madrid, akiwa mfungaji bora wa ligi ya Uhispania na Ligi ya Mabingwa.
Alifunga mabao 44 akiwa na Madrid, yakiwemo 15 katika mashindano makubwa ya Uropa, na kumfikia Raúl González kama mfungaji wa pili kwa wingi wa mabao katika klabu hiyo nyuma ya Cristiano Ronaldo.
Naye mchezaji wa Uhispania Alexia Putellas alishinda Ballon d’Or kwa upande wa wanawake kwa mwaka wa pili mfululizo kufuatia msimu mwingine bora kabisa na timu ya Barcelona.