KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake chini ya miaka 17, Serengeti Girls jana kilipata ushindi wa kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia.
Michuano hiyo inaendelea nchini India ambapo ushindani umekuwa mkali kwa kila timu ambazo zinashuka uwanjani ndani ya dakika 90 kusaka ushindi.
Ni ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ufaransa ilifanikiwa kushinda chini ya Kocha Mkuu, Bakari Shime.
Utulivu mkubwa kwa Serengeti Girls uliwapa ushindi huo wa kwanza ikiwa ni mchezo wao wa pili katika kundi D baada ya mchezo ule wa kwanza kuambulia kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya Japan.
Ni Diana Mnaly alipachika bao dakika ya 17 lile la ushindi ni mali ya Christer Bahera dakika ya 60 kwa mkwaju wa penalti huku lile la Ufaransa likifungwa na Lucie Calba kwa penalti.
Pia mchezo huo Serengeti Girls ilimaliza ikiwa pungufu baada ya Joyce Lema kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 90 imebakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Canada katika kundi D unaotarajiwa kuchezwa Jumanne nchini India.