FISTON Mayele mshambuliaji namba moja ndani ya kikosi cha Yanga anaingia kwenye dakika 90 za moto kushirikiana na mastaa wengine kupata matokeo ugenini kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal.
Katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Oktoba 8, ubao uliposoma Yanga 1-1 Al Hilal ni Mayele alifunga kwa Yanga na kumfanya afikishe mabao 7 katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kuwa ni kazi kubwa ambayo wanayo ugenini ili kushinda ni lazima washambuliaji kufunga kwa kila nafasi watakazopata.
“Kwa nafasi ambazo tutapata nimewaambia wachezaji ni muhimu kuzitumia kwa umakini mkubwa na hilo litatufanya tushinde, sio Mayele, (Fiston) bali wachezaji wote kazi ni moja kusaka ushindi.
“Ugenini mchezo wetu utakuwa mgumu hasa ukizingatia wapinzani wetu kwenye mechi zao ambazo huwa wanacheza nyumbani hawapendi mbinu zao kuonekana kama ambavyo walifanya dhidi ya St George,” amesema Nabi.