STARS WAPENI TABASAMU WATANZANIA

 HAIKUWA bahati kwa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kupata ushindi kwenye mechi za kuwania kufuzu CHAN baada ya kupoteza kwenye mchezo dhidi ya Uganda kwenye mchezo wa nyumbani na ugenini.

Kwa sasa wachezaji 23 wameitwa kikosi cha timu ya Taifa kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Libya na huu upo kwenye kalenda ya FIFA.

Mechi mbili za kirafiki zinatarajiwa kuchezwa hivyo wachezaji wana kazi nyingine ya kusaka ushindi kwenye dakika 180 zijazo ambazo hazitakuwa nyepesi.

Tumeambiwa kwamba wachezaji hawa walioitwa ni chaguo la awali na wapo wengine ambao wataongezwa kwenye kikosi hivyo wote waliotwa na ambao hawajaitwa wana kazi ya kurejesha tabasamu kwa Watanzania.

Kinachohitajika ni matokeo mazuri kwenye mechi zote na inawezekana ikiwa wachezaji watakuwa makini na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi.

Kikubwa ni kukubali kufundishika na kuelewa kwamba kila kitu kinawezekana na ambacho wanahitaji Watanzania ni furaha kupitia matokeo mazuri.

Imani yetu ni kuona kambi itakapoanza kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye kila eneo kuanzia safu ya ushambuliaji na ulinzi malengo yakiwa ni kushinda mechi zote.

Unaweza kusema labda kwa kuwa ni mechi za kirafiki hazina umuhimu hapana hizi ni mechi za umuhimu na FIFA wenyewe wanazifuatilia kwa ukaribu.

Kila la kheri kwa wachezaji mlioitwa na wale ambao mtaitwa hapo baadaye wakati wa tabasamu ni sasa.