KIKOSI cha Azam FC, kesho Septemba 12 kinatarajia kuibukia Mbeya kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuikabili Mbeya City, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 13.
Huo utakuwa ni mchezo wa tatu kwa Azam FC kucheza ndani ya ligi kwa msimu wa 2022/23 baada ya kukamilisha mechi tatu.
Mechi mbili walicheza Uwanja wa Azam Complex na walicheza mchezo mmoja ugenini dhidi ya Yanga, Uwanja wa Mkapa na walitoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2.
Kali Ongala, kocha wa washambuliaji ndani ya Azam FC amebainisha kuwa mpango mkubwa ni kupata matokeo kwenye mechi ambazo tutacheza.
“Tunatambua kwamba ligi ni ngumu na kila timu inahitaji ushindi nasi tunajitahidi kupata kile ambacho tunastahili, kikubwa ni kutumia nafasi ambazo tunapata hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” amesema.
Ikiwa imecheza mechi tatu Azam FC imekusanya pointi 5, ilishinda mechi moja, sare mbili huku ile safu ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao matano.
Kinara wa utupiaji ni Tepsi Evance ambaye amefunga mabao mawili ndani ya Azam FC na ana pasi moja ya bao.