YANGA KAMILI KUIVAA ZALAN FC KWA MKAPA

 CEDRICK Kaze, Kocha Msaidizi wa Yanga ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Zalan FC unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, leo Septemba 10,2022.

Yanga inaingia katika mashindano haya ikiwa na kumbukumbu ya kutolewa katika hatua ya awali michuano hiyo msimu uliopita wa 2021/22.

Ni Klabu ya Rivers United iliweza kushinda mechi zote mbili nje ndani jambo lililowafanya Yanga kufungashiwa virago jumlajumla.

Kaze amesema:”Tunatambua kwamba utakuwa mchezo mgumu na kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya kupata matokeo kwenye mchezo wetu.

“Ni deni kwetu kwa kuwa ninajua kwamba msimu uliopita hatukufanya vizuri hivyo msimu huu tunajukumu la kupambana kufanya vizuri ili kusonga mbele kwenye mashindano haya,” amesema.

Jana kikosi cha Yanga kilifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo na miongoni mwa wachezaji waliokuwa mazoezini ni pamoja na kiungo Dennis Nkane, Bakari Mwamnyeto, Zawad Mauya na Yannic Bangala.