KIUNGO WA KAZI SIMBA AINGIA KWENYE VITA

SADIO Kanoute raia wa Mali, kiungo wa kazi ngumu ndani ya kikosi cha Simba ameingia kwenye vita nyingine na mastaa wengine wawili wa kikosi cha timu hiyo kuwania tuzo.

Ni tuzo ya mchezaji bora chaguo la mashabiki ndani ya Simba inayopatikana kutokana na mashabiki wa timu hiyo ambayo imeweka kambi nchini Sudan kupiga kura.

Kanoute kwenye mechi anazocheza huwa hana bahati ya kumaliza dakika atakazopewa bila kupitisha mikato yake ya kimyakimya kwa wapinzani wake.

Kwenye mechi zake mbili za ligi alizocheza msimu huu wa 2022/23 akiyeyusha dakika 180 alicheza jumla ya faulo nne, akionyeshwa kadi moja ya njano kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar dakika ya 62.

Wengine ambao anawania nao tuzo hiyo ni kiungo Pape Sakho raia wa Senegel mzee wa kunyunyiza pamoja na kiungo Clatous Chama raia wa Zambia.

Rekodi zinaonyesha kuwa Chama ambaye amecheza mechi mbili za ligi na kufunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar ana nafasi kubwa ya kusepa na tuzo hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Emirate Aluminium.