>

MWAMBA HUYU KUCHUKUA MIKOBA YA SAKHO SIMBA

 JEAN Morel Poé,anatajwa kuwa kwenye hesabu za mabosi wa Klabu ya Simba wakiangalia uwezekano wa kumsajili endapo tu Pape Ousmanne Sakho atauzwa kwenda Wydad Casablanca ya Morocco inayomuhitaji baada ya kumuwekea ofa ya shilingi bilioni 1.6.

 Sakho ambaye baada ya kushinda Tuzo ya Bao Bora la Mwaka CAF vigogo kibao wameanza kumnyemelea, Simba hawakutaka kuchelewesha, mapema tu wameanza kumsaka mbadala wake ambaye anatajwa kuwa ni mwamba huyo raia wa Ivory Coast.

Poé anayemudu vizuri kucheza winga zote kama ilivyo kwa Sakho, lakini ameongezewa uwezo pia wa kucheza kiungo mshambuliaji wa kati na straika wa mwisho kwa maana ya namba tisa.

Chanzo cha uhakika kutoka katika Kambi ya Simba iliyopo Mji wa Ismailia nchini Misri, kimesema kwamba uongozi wa klabu hiyo upo kwenye majadiliano mazito juu ya kumsajili mwamba huyo anayewachezea Waarabu wa Misri, timu ya Ismailia.

Mtoa taarifa huyo amesema Kocha Zoran Maki ndiye amependekeza Poé asajiliwe baada ya kumuona wakati wa mechi ya kirafiki walioyocheza dhidi ya Ismailia na kutoka sare ya bao 1-1.

“Huyu jamaa siyo straika moja kwa moja, ni mtu wa pembeni, tulicheza naye mechi ya kirafiki ile dhidi ya Ismailia tuliyotoka sare ya 1-1.

“Ni mchezaji mzuri sana, watu walivutiwa naye, ukiangalia kikosini kwetu kwa sasa tuna wachezaji wa pembeni wengi, lakini uongozi unaangalia namna ya kumsajili kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zote za mbele ikiwemo mshambuliaji wa mwisho.

“Bado ana mkataba na Ismailia, amesajiliwa na timu hiyo Januari mwaka huu, tusubiri uongozi utafikia wapi kuhusu dili lake kwani bado wanaendelea kujadiliana,” alisema mtoa taarifa huyo.

 Usajili wa Poé endapo ukikamilika, basi mchezaji huyo atawapa vitu vingi Simba kutokana na namna mfumo wa Kocha Zoran Maki ataamua kuutumia kulingana na mechi husika kwa sababu ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja eneo la ushambuliaji.

Hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema: “Suala la usajili bado linaendelea, kila ukikamilika tutaweka wazi.