CRDB WAFURAHIA TUZO,WAIREJESHA KWA WATEJA

MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori amefurahia tuzo ya ‘Benki Bora Tanzania’ na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, pamoja na Meneja Mipango ya Biashara Benki ya CRDB Masele Msita.

Furaha ya viongozi hao ilikuwa katika hafla ya kuwashukuru wateja na wadau wa Benki hiyo kwa mafanikio hayo iliyofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB Jijini Dar es Salaam  20 Julai 2022.

Jarida maarafu la fedha na uchumi la Euromoney liliitaja Benki ya CRDB kama moja ya benki bora duniani katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa benki zilizofanya vizuri iliyofanyika Julai 13 2022 Jijini London nchini Uingereza.

Shukrani hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB na kuhudhuriwa na wajumbe wa bodi, wafanyakazi na wateja wa Benki hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam, Nsekela amesema wateja wa benki hiyo wamekuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa mkakati wa mageuzi ya biashara ambao umepelekea kupata tuzo hiyo.

“Niwashukuru wateja, wanahisa, Serikali, Benki Kuu ya Tanzania na washirika wetu wa biashara kwa ushirikiano wanaotupa na kuendelea kutufanya kuwa bora zaidi. Hii sio tuzo ya Benki ya CRDB peke yake, ni tuzo ya Watanzania wote,” amesema Nsekela.

Mwaka 2019, Benki hiyo ilianza ikifanya mageuzi katika biashara yake ambayo yamejikita katika kutengeneza thamani endelevu, kuongeza ujumuishi wa kifedha na kujenga uchumi jumuishi kupitia bidhaa, huduma, na mifumo bunifu ya utoaji huduma.

Tuzo ya Euromoney inathibitisha nafasi ya Benki ya CRDB kama ‘Benki Kiongozi’ nchini. Vilevile, inatambua mafanikio ya mageuzi haya ambayo yamepelekea ukuaji endelevu wa Benki yetu na ukinufaisha wateja, wawekezaji na uchumi wa nchi kwa ujumla wake.

Waandaji wa tuzo hizo pia wametambua mchango wa mageuzi wa kidijitali ambayo yamefanyika ndani ya Benki ya CRDB, ikielezwa kuwa kiasi kikubwa yamesaidia kuchochea ongezeko la ujumuishi wa kifedha nchini.