BEKI APEWA MKATABA MGUMU AKUBALI KUSAINI JANGWANI

MABOSI wa Yanga wamempa mkataba mgumu wa mwaka mmoja wenye masharti beki wake wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ hiyo ikiwa ni siku chache tangu beki huyo atambulishwe kuendelea kubakia kuichezea timu hiyo.

Awali, beki huyo alikuwa katika mipango ya kuachwa pamoja na baadhi ya wachezaji akiwemo Yassin Mustapha, Deus Kaseke na Paul Godfrey ‘Boxer’.

Taarifa zimeeleza kuwa beki huyo amekubali kusaini mkataba huo wenye sharti la kuonyesha kiwango bora ndani ya msimu huo mmoja aliopewa.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa beki huyo ametakiwa kupambania namba katika kikosi cha kwanza na kama akishindwa basi upo uwezekano mkubwa wa kuachwa mara baada ya huo aliouongeza kumalizika.

Aliongeza kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia Nasreddine Nabi ndiye aliyempendekeza na lengo ni kumpa nafasi ya kuonyesha kiwango chake baada ya msimu huu uliomalizika kusumbuliwa na majeraha.

“Nafasi ya mwisho amepewa Ninja, ni baada ya kocha Nabi kupendekeza kuongezewa mkataba wa mwaka mmoja pekee.

“Amepewa nafasi ya kujiuliza kwa kupambania nafasi ya kucheza na kuonyesha kiwango chake katika msimu ujao, kama unavyofahamu msimu huu uliomalizika alisumbuliwa na majeraha ya goti.

“Majeraha hayo yalimsababishia afanyiwe oparesheni ya goti ambayo yamepona, hivyo amepewa nafasi ya kuonyesha kiwango bora kwa kipindi hicho, hiyo ndio sababu ya kupewa mkataba huo mfupi,” alisema mtoa taarifa huyo.

Rais wa timu hiyo, Injinia Hersi Said alizungumzia usajili huo kwa kusema: “Ninja ni kati ya wachezaji waliobakia kuipambania timu yetu ya Yanga, na kikubwa anatakiwa kuonyesha ubora wake msimu ujao.”