SUALA LA MKATABA KUVUNJWA KYOMBO LAFAFANULIWA

MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Singida Big Stars iliyo na maskani yake mkoani Singida Hussein Massanza amesema kuwa mchezaji aliyesajiliwa na klabu hiyo kutoka Klabu ya Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja Habibu Kyombo ameiomba klabu hiyo kuvunja mkataba kutokana na kuwa na malengo makubwa zaidi.

Meneja huyo amebainisha kuwa Kyombo alitoa sababu ambazo kimsingi mwanzo zilikuwa ni ngumu kwa klabu kukubaliana naye lakini baadaye waliangalia maslahi mapana ya klabu na mchezaji ambapo hekima ilitumika na mkataba ukavunjwa rasmi.

Amesisitiza pia kuwa Menejimenti ya Habibu Kyombo ilitekeleza taratibu zote zinazotakiwa kufanyika ili kuvunja mkataba na kwa kufanya hivyo pande zote mbili zilikubaliana na hatimaye kama klabu kumtakia Kyombo mkono wa kwaheri.

Juni 22 alitambulishwa rasmi ndani ya Singida Big Stars kisha Julai 4 ilitolewa taarifa kuhusu kusitisha mkataba wa mchezaji huyo.

Aidha amesisitiza kuwa Kyombo wakati anasajiliwa halikuwa pendekezo la kocha bali ni Kamati ya Usajili ya Klabu hiyo ndiyo ilimsajili kwa kuangalia sifa zinazofanana na zile za mapendekezo ya kocha.

Kwa upande mwingine Meneja huyo wa Habari na Mawasiliano amebainisha kuwa Singida Big Stars inafanya usajili wa kuhakikisha msimu ujao inaingia katika mbio za Ligi Kuu kusaka nafasi nne za juu ikiwa na lengo la kushiriki katika mashindano ya kimataifa.