MABINGWA wa Ligi Kuu ya Uingereza Klabu ya Manchester City imetangaza kukamilisha dili la kumsaini kiungo mkabaji wa Klabu ya Leeds United raia wa Uingereza Kalvin Phillips kwa mkataba wa miaka 6 ambao unatarajiwa kumalizika majira ya joto mwaka 2028.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 amesajiliwa kwa kiasi cha paundi milioni 45 ambazo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 127.5 za kitanzania, na amekabidhiwa jezi namba 4 ikiwa ni baada ya kuitumikia klabu yake ya utotoni ya Leeds United kwa kipindi cha miaka 8.
Usajili wa Phillips unakuwa ni usajili wa tatu kufuatia kutua kwa mshambuliaji raia wa Norway Erling Braut Haaland kutoka Borussia Dortmund pamoja na golikipa Stefan Ortega ikiwa ni maandalizi ya msimu ujao.
Mara baada ya kujiunga na Manchester City Phillips amesema:“Kiukweli najisikia faraja sana kujiunga na klabu ya Manchester City ambayo ni moja ya timu bora katika Ligi Kuu ya Uingereza lakini pia ikiongozwa na Pep Guardiola ambaye kimsingi ni moja ya makocha bora Duniani.”
Phillips ni moja ya wachezaji waliokuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Uingereza chini ya Kocha Gareth Southgate kilichofika Fainali za Kombe la Euro 2020 huku akiwa na jumla ya michezo 23 katika ngazi ya Timu ya Taifa.