KOCHA MPYA SIMBA ANAAMINI WATASHINDA VITU VINGI

KOCHA mpya wa Simba,Zoran Manojlovic ameweka wazi kuwa anaamini kwamba atarejesha heshima ndani ya kikosi hicho atakapoanza kazi.

Ilikuwa Mei 28 ambao Simba ilimtangaza Zoran kuwa kocha wa Simba akipokea mikoba ya Pablo Franco ambaye alifutwa kazi.

Ilikuwa ni Mei 31 mwendo wa Pablo uligota ukingoni msimu wa 2021/22 baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.

Kocha huyo ambaye amesaini dili la mwaka mmoja amesema:”Nashukuru kwa nafasi ambayo nimepata kuiongoza Klabu ya Simba kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao,najua hii ni klabu kubwa na ina mashabiki wengi wanapenda kuona inafanya vizuri.

“Ninatumaini kwamba nitapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwenu na tutakuwa na mafanikio makubwa na tutashinda vitu vingi kwa pamoja,” amesema.

Kwenye msimamo Simba imemaliza ikiwa nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 30 msimu wa 2021/22 ikiwa na pointi 61.