UNAAMBIWA Yanga SC ilimshusha kimyakimya beki raia wa DR Congo, Joyce Lomalisa Mutambala na kumpa mkataba wa miaka miwili, huku kwa mwezi akitarajiwa kulipwa shilingi milioni sita.
Kwa muda wa miaka miwili akiwa anaitumikia Yanga, jumla atakuwa amepokea mshahara wa shilingi milioni 144 hadi kumalizika kwa mkataba wake.
Mutambala anajiunga na Yanga akitokea Bravos do Maqui ya Angola, pia amewahi kucheza GD Interclube (Angola), AS Vita (DR Congo) na Mouscron ya Ubelgiji.
Chanzo chetu kutoka Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, Mutambala alikuwa hapa nchini kwa takribani wiki moja kukamilisha usajili wake huo ambapo baada ya kusaini, akarudi kwao DR Congo.
“Naomba nikueleze kuwa, kuna uwezekano mkubwa sana kwa Kocha Nasreddine Nabi kuwaondoa kwa mkopo mabeki wa kushoto, David Bryson na Yassin Mustafa kwa sababu tayari dili la beki wa kimataifa raia wa DR Congo, Lomalisa Mutambala limekamilika.
“Mutambala alikuja hapa nchini kama wiki moja iliyopita, akasaini mkataba wa miaka miwili, kisha akaondoka. Atakuwa akilipwa mshahara wa shilingi milioni 6.
“Baada ya kusaini na kurudi kwao, ametakiwa kurejea nchini mapema zaidi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya,” kilisema chanzo hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Saidi, hivi karibuni alisema wamepanga kufanya usajili mkubwa kuiandaa timu hiyo ili ifanye vizuri katika michuano ya kimataifa na ile ya ndani kwa msimu ujao wa 2022/23.