YANGA SC wanataka kuzifundisha timu nyingine namna gani ya kushangilia ubingwa msimu huu, hiyo ni baada ya Msemaji wa Yanga, Haji Manara kuweka wazi kwamba wameagiza gari maalumu la kubeba wachezaji na kutembeza kombe lao.
Manara anasema, basi ambalo wameagiza ni kama lile walilolitumia Real Madrid kushangilia ubingwa wao wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2021/22.
Yanga tayari wameshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na wanatarajiwa kukabidhiwa kombe hilo Jumamosi hii katika mchezo dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Akizungumza jinsi ambavyo Yanga watalitembeza kombe lao, Manara alisema: “Lazima tuwafundishe timu nyingine jinsi gani ya kuushangilia ubingwa wa ligi kuu.
“Tayari tumeshaagiza gari maalumu kwa ajili ya kuushangilia ubingwa huo, gari hilo linafanana na ambalo walilitumia Real Madrid na Liverpool kushangilia makombe ambayo waliyabeba msimu huu.
“Kuhusu utaratibu, mashabiki wote wa Yanga Jumapili tunawakaribisha uwanja wa ndege kwa ajili ya kuushangilia ubingwa na kutembeza kombe ambapo tutatoka uwanjani hapo, tutaelekea katika Makao Makuu ya Klabu pale Kaunda Jangwani, tutapitia Msimbazi,” alisema Manara.