SIMBA YAMUACHIA STRAIKA WAO KUTUA SINGIDA

IMEELEZWA kuwa, Simba ipo katika mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kumuachia mshambuliaji wake, Yusuph Mhilu kwenda Singida Big Stars.

Mhilu ni kati ya washambuliaji waliosajiliwa na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu, kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao ambacho kimeshindwa kutetea mataji yake ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Singida tayari imeanza kufanya usajili kuelekea msimu ujao na baadhi ya nyota ikiwatambulisha akiwemo mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Habibu Kyombo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, tayari mazungumzo yameanza kati ya Simba na Singida kwa ajili ya kumsajili Mhilu kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Mtoa taarifa huyo alisema Simba ndio wamependekeza kumuachia mshambuliaji huyo kwenda huko kwa mkopo kwa ajili ya kupata nafasi kubwa ya kucheza.

“Simba huenda ikamuachia kwa mkopo Mhilu kwenda Singida ambayo imeonesha nia kubwa ya kumuhitaji kwa ajili ya msimu ujao.

“Tayari Singida imeanza mazungumzo ya kimyakimya na mshambuliaji huyo kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo.

“Mhilu hakuwa na msimu mzuri Simba tangu alipotoka Kagera Sugar hali inayowafanya mabosi wa Singida kutumia mwanya huo kumshawishi kuitumikia timu yao japo kwa mkopo,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mtendaji Mkuu wa Singida, Muhibu Kanu, juzi alizungumzia usajili wao kwa kusema: “Tumepanga kufanya usajili wetu wa kimyakimya ambao tutauweka wazi mara baada ya taratibu zote kukamilika. Hiyo ni baada ya kutangaza wachezaji tuliowaacha.”