KAMBOLE AOMBA JEZI NAMBA 7 YANGA

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Zambia ambaye ni ingizo jipya ndani ya Yanga, Lazarous Kambole, amesema kuwa angependa kutumia jezi namba 7 ndani ya Yanga huku akiweka wazi kuiomba jezi hiyo kwa matumizi ya msimu ujao akiamini kuwa ni namba ambayo anaipenda.

Kwa upande wa Yanga, jezi namba 7 ilikuwa ikitumiwa na Balama Mapinduzi ‘Kipenseli’, ambaye huenda akatolewa kwa mkopo kutokana na kutokutumiwa sana na kocha Nassredine Nabi katika siku za hivi karibuni, licha ya kuwa na majeruhi.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kambole alisema kuwa anatamani kupata jezi namba saba ndani ya Yanga jambo ambalo anasubiri kuona kama atapewa kwa ajili ya matumizi ya msimu ujao na kama itashindikana basi atachagua jezi yoyote itakayopatikana.

“Napenda ipatikane jezi namba saba kwa kuwa ni jezi ambayo nilikuwa nikiivaa mara kwa mara ndani ya timu ya taifa ambapo pia nilikuwa nikifanya vyema lakini kama itashindikana basi nitachagua jezi nyingine yoyote ambayo itapatikana.

“Kwa sasa hayo mambo ya jezi bado kwa kuwa msimu bado haujamalizika lakini nadhani tukianza maandalizi ya msimu ujao basi kila kitu kitafahamika ila namba saba kwangu ni chaguo langu la kwanza,” alisema mchezaji huyo.