MSHAMBULIAJI wa Klabu ya Real Madrid Rodrygo Silva de Goes maarufu kama Rodrygo amebainisha kuwa wachezaji wa Real Madrid walipanga kumdhihaki mshambuliaji wa Liverpool na Timu ya Taifa ya Misri Mohamed Salah mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya maarufu kama Uefa.
Mshambuliaji huyo amenukuliwa akisema:“Pale inapotokea mtu anakukashfu kuna muda unatamani kushinda ili umdhihaki, kwenye mazoezi tulikuwa tukisema kazana Salah! kazana Salah!.
Katika vichwa vyetu tayari tulikuwa tunawaza lazima tushinde ili tumdhihaki Salah. Aliendelea kwa kusema: “Baada ya fainali kumalizika tulipishana na wachezaji wa Liverpool katika korido Salah alikuwa anahuzunika sana ambapo (Luka) Modric alimuambia “Jaribu tena wakati mwingine.”
Ikumbukwe kuelekea Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo Real Madrid ilishinda na kunyakua kombe lake la 14 la Ligi hiyo, Salah alisema anatamani kukutana na Real madrid ili aweze kulipa kisasi kutokana na kuumizwa bega na Sergio Ramos katika Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya iliyofanyika mwaka 2018 ambayo Liverpool ilipoteza kwa jumla ya mabao 3-1.