AZIZ KI, MORRISON WAIPA JEURI YANGA

SI unauona moto walionao mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu Yanga SC? Sasa unaambiwa uongozi wa timu hiyo umetamba kuwa kwa usajili ambao wanaendelea kuufanya, basi watu wanapaswa kufahamu wanachokiona kwa sasa ni robo tu ya ubora ambao kikosi chao kitakuwa nao msimu ujao.

Kuelekea msimu ujao wa 2022/23, Yanga wameanza kufanya maboresho ya kikosi chao, ambapo mpaka sasa wamekamilisha usajili na kumtangaza mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Lazarous Kambole.

Ukiachana na Kambole, mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu Bara wanatajwa kuwa tayari wamemalizana na mastaa wengine wakiwemo aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa ASEC Mmosas, Stephane Aziz Ki na kiungo wa Simba, Bernard Morrison.

Akizungumza na Spoti Xtra, kuhusu usajili wa kikosi chao, Msemaji wa Yanga, Haji Manara alisema: “Tayari tumeshaanza mchakato wa kufanya maboresho ya kikosi chetu kwa ajili ya msimu ujao na kupitia mapendekezo ya kocha Nabi (Nasreddine) tumeanza kutambulisha wachezaji wapya.

“Tumeweka wazi kuwa tutafanya usajili wa mastaa wanne au watano, niwahakikishie kuwa huu moto tulionao msimu huu ni robo tu ya ubora wa kikosi tutakachokuwa nacho msimu ujao, hivyo wapinzani wetu wajiandae.”