SAKATA la usajili wa kiungo mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Stephen Aziz Ki, limezidi kuteka hisia za wapenda soka wengi hapa nchini, baada ya vigogo Simba SC na Yanga SC kuhusishwa naye.
Kiungo huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto awapo uwanjani, inaelezwa kwamba tayari amemalizana na Yanga ambayo imetumia kiasi cha shilingi milioni 650 kumpa mkataba wa miaka miwili.
Nyota huyo wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, awali alikuwa akitajwa zaidi kutakiwa na Simba ambayo yenyewe inaelezwa kumuwekea ofa ya mkataba wa miaka miwili kwa mshahara wa dola 10,000 (sawa na Sh 23,224,041 za Kitanzania) kwa mwezi, huku ada ya uhamisho ikiwa ni dola 140,000 (sawa na Sh 325,136,578 za Kitanzania)
Yanga katika usajili wa msimu ujao tageti yao namba moja ipo kwa Aziz Ki ambaye anakuja kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kwa timu hiyo itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga, kimeeleza kuwa, klabu hiyo imewalazimu kutumia kiasi kisichopungua shilingi milioni 650 katika kukamilisha dili la mchezaji huyo.
Mtoa taarifa huyo alienda mbali zaidi na kusema mchezaji huyo amewekewa mshahara mkubwa kuliko mchezaji yeyote ndani ya Yanga kulingana na makubaliano yaliyopo.
“Yanga imetulazimu kutumia kiasi kisichopungua shilingi milioni 650 kumsajili Aziz Ki na hiyo ni kulingana na ubora wa mchezaji huyo ambaye anahitajika na timu nyingi.
“Hilo limefanya tusiwe na sababu zaidi ya kutimiza kile anachokihitaji ili tu tumsajili.
“Yanga tunahitaji kufanya vema katika usajili wa kimataifa msimu ujao, hivyo lazima tuhakikishe tunapambana kusajili wachezaji wa maana ambao watatufanya tuendelee kuwa bora.
“Ukiachana na Aziz Ki, pia kuna wachezaji wengine wa maana watasajiliwa, lengo ni kufanya vema katika michuano ya kimataifa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande mwingine, kupitia Mtandao wa Kijamii wa Instagram Aziz Ki amemtumia ujumbe nyota wa Yanga, Yacouba Songne akimwambia muda si mrefu watakutana Tanzania.
Aziz Ki aliandika ujumbe huo ulioambatana na picha akiwa na Yacouba na mchezaji mwingine wa Burkina Faso wakishika jezi za Yanga uliosomeka hivi; “Kaka Yacouba Songne, muda si mrefu tutaonana.” Kisha akasindikiza na bendera ya Tanzania na alama za kopa zenye rangi ya kijani.
Yacouba naye alimjibu kwa kusema: “Karibu sana.” Jambo ambalo linaashiria kuwa Yacouba anamkaribisha nyota huyo ndani ya Yanga.