UONGOZI wa Singida Big Stars imeweka wazi kuwa unatambua ubora wa beki wa Simba, Pascal Wawa ila haina mpango wa kumsajili kwa muda huu.
Timu hiyo ambayo ilikuwa inaitwa DTB ilipokuwa inashiriki Championship inatajwa kuwa katika mazungumzo na Wawa ambaye mkataba wake unakaribia kuisha msimu utakapomeguka.
Mtendaji Mkuu wa Singida Big Stars,Muhibu Kanu amesema kuwa mipango ya usajili ipo na watasajili wachezaji wazuri kwa malengo.
“Tuna mpango wa kufanya usajili mzuri kwa malengo kwa kutumia ripoti ya benchi la ufundi lakini suala la kumsajili Wawa, (Pascal) kwa sasa halipo kwenye mpango wetu.
“Mimi ninahusika kwenye masuala ya usajili hivyo ni suala la kusubiri ripoti inaeleza nini na inahitaji kitu gani kumbuka kwamba tumetoka kukamilisha kazi ya kupanda kutoka Championship na sasa tupo kwenye ligi lazima tujiandae,” amesema Kanu.