LIGI KUU ENGLAND KUFIKA TAMATI LEO,MBIVU NA MBICHI KUJULIKANA

MBELE huko Premier League inaenda kumalizwa hivi kukiwa na vita tatu kali, majibu yake yatapatika baada ya dakika tisini kutimia za mechi hizo.

UBINGWA

Bingwa wa Premier League atafahamika leo kama ni Manchester City au Liverpool. Man City wataingia uwanjani kuvaana na Aston Villa kwenye Uwanja wa Etihad.

Man City ni vinara wa Premier wakiwa na pointi 90, wamewaacha Liverpool walio nafasi ya pili kwa pointi moja. Ushindi unahitaji kwa Man City ili kutetea ubingwa wao.

Liverpool wanaomba Man City wapoteze, kisha wao waifunge Wolves ili ibebe ubingwa. Kwenye mabao, Man City imefunga 96 na kuruhusu 24.

Liverpool wakiwa na pointi 89, wanamaliza ligi Anfield dhidi ya Wolves. Wamefunga mabao 91 na kuruhusu 25.

TOP FOUR

Hii ni vita nyingine, tayari Man City, Liverpool na Chelsea, zimejihakikishia kumaliza ndani ya nne bora, imebaki nafasi moja inayowaniwa na Tottenham na Arsenal.

Wakati wakiingia katika mchezo wa leo, Tottenham wenye pointi 68, wanaenda kuvaana na Norwich City ambao wameshuka daraja tayari, wanahitaji sare tu ili kumaliza nafasi ya nne na kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arsenal walio nafasi ya tano, wanamaliza nyumbani dhidi ya Everton, kwa sasa wana pointi 66. Kazi kubwa kwa Arsenal ni kuicheza mechi yao kupata ushindi, kisha kuomba Tottenham ipoteze, yani hata sare si salama kwao.

Tottenham mara ya mwisho kumaliza ndani ya nne bora ilikuwa msimu wa 2018/19, Arsenal ilikuwa msimu wa 2015/16 ikimaliza nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Leicester City.

KUSHUKA DARAJA

Katika eneo hili ambalo ni gumu kabisa, tayari Norwich City na Watford wameshuka daraja.

Sasa mechi za leo, Leeds United au Burnley mmoja wapo lazima ataondoka ndani ya Premier League.

Kumbuka Leeds United mechi ya mwisho anacheza na Brentford ugenini, huku Burnley akicheza na Newcastle United.

Wawili hawa kila mmoja ana pointi 35, lakini wametofautiana mabao ya kufunga na kufungwa. Burnley yupo juu ya Leeds. Kila mmoja anamuombea mabaya mwenzake, zaidi Leeds anaomba ashinde, kisha mwenzake afungwe au apate sare ili yeye abaki salama.