KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesema kuwa watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Azam FC ili kuendelea kukusanya pointi nyingi zaidi.
Simba leo Jumatano wanatatarajiwa kucheza na Azam FC katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi kuu utakaofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar.
Simba wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi walioupata dhidi Azam katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa mabao 2-1 uliofanyika katika Uwanja wa Mkapa.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kocha Franco alisema kuwa japo mchezo ni mgumu lakini watapambana kuhakikisha kuwa wanapata matokeo ambayo yatawafanya kutoachwa pointi nyingi dhidi ya wapinzani wao, Yanga.
“Tunafahamu kuwa Azam ni timu nzuri hivyo tunatarajia kupata upinzani mkubwa kutoka kwao hivyo mchezo hautakuwa rahisi bali utakuwa ni mgumu hivyo tunatakiwa kupambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.
“Matokeo ya mchezo uliopita yalikuwa mazuri kwa upande wetu lakini tulipata upinzani mkubwa sana kwao hivyo naona hata mchezo huu ukiwa hivyo lakini kwa maandalizi tuliyoyafanya tunaamini kuwa tupo tayari kwa mechi,” alisema kocha huyo.
Kwa upande wa Kocha wa Makipa wa Azam FC, Mwalo Hashim alisema kuwa: “Baada ya kukosa matokeo katika michezo mitatu mfululizo dhidi ya Simba katika Uwanja wa Azam Complex safari hii tumejipanga kuhakikisha kuwa tunashinda ili kuvunja rekodi hiyo, tunafahamu kuwa haitakuwa rahisi lakini tutajitoa ili tushinde.”
KUHUSU UBINGWA
Kuhusu timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu, Pablo amesema: “Bado tunapambana kuhakikisha kuwa nini kitatokea huko mwishoni haswa kwenye suala la ubingwa ambalo lipo mikononi mwa Yanga ambao kama watafanya vibaya basi tunaweza kuipata nafasi hiyo.
“Japo tunaona ni ngumu kutokana na ubora wa Yanga lakini tunatakiwa kushinda michezo yetu hatuwezi kujua nini kitatokea.”
Waandishi: Marco Mzumbe, Kilima Mohammed, Angela Mmbaga, Flora Kaiza na Silvia Chalamila