UNAWEZA kusema mwenendo wa ufungaji wa washambuliaji wa Simba msimu huu, hauwafurahishi wengi ndani ya klabu hiyo, hali iliyomfanya Rais wa Heshima, Mohamed Dewji kuweka zaidi ya shilingi milioni 800 za usajili msimu ujao.
Mo alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kabla ya kuachia nafasi hiyo kwa Salim Abdallah ‘Try Again’, huku yeye akipewa cheo cha Rais wa Heshima klabuni hapo.
Simba ambayo msimu huu safu yake ya ushambuliaji imeonekana kuyumba kulinganisha na msimu uliopita, mabosi wa timu hiyo wameamua kuingia chimbo kusaka majembe mapya.
Timu hiyo iliyoshiriki michuano ya kimataifa msimu huu, ilishindwa kufurukuta kuanzia Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoishia hatua ya kwanza, kabla ya kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika na kuishia robo fainali.
Chanzo chetu kutoka Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, Mo Dewji amelazimika kutoa fedha hizo ili kusaidia usajili kwenye dirisha lijalo.
Mtoa taarifa huyo aliongeza kwamba, Mo amewataka viongozi wa usajili wa klabu hiyo kuhakikisha wanatafuta washambuliaji wenye sifa zitakazoendana na mashindano yajayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Mo ameamua kutoa zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuhakikisha tunapata washambuliji wa kimataifa wenye uwezo mkubwa.
“Tuna imani kama tutabahatika kufanikiwa kupata washambuliaji hao, basi maboresho ya masimu ujao yatakuwa ya kipekee na kwamba Simba itakuwa moto wa kuotea mbali katika mashindao yote.
“Ngoja nikwambie tu ukweli, katika majadiliano yetu, tulipanga kuachana na mastraika wetu wote, maana tunaona kama uwezo wao ni wa ndani tu na siyo kwa malengo yetu ya kimataifa.
“Baada ya fedha hizo kutolewa, muda si mrefu mtaanza kuona vyuma vinashushwa kwa ajili ya kuimarisha timu,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema msimu ujao kikosi chao kitakuwa imara zaidi kwa lengo la kufanya vizuri michuano yote watakayoshiriki.
Ikumbukwe kuwa, katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Simba imefunga mabao 31, huku kinara wao akiwa Meddie Kagere mwenye saba.