ISHU YA MORRISON KUIBUKIA YANGA,SIMBA WATOA TAMKO

BERNARD Morrison kiungo wa kikosi cha Simba anatajwa kuwa kwenye hesabu za kurejea ndani ya kikosi cha Yanga ambacho alicheza hapo kabla ya kujiunga na mabingwa hao watetezi.

Morrison kwa hivi karibuni amekuwa nje ya uwanja kwa muda huku Kocha Mkuu, Pablo Franco akibainisha kwamba ambacho kinamuweka nje nyota huyo ni majeruhi.

Mkataba wake unatarajia kufika ukingoni pale ligi itakapoisha na hakuna taarifa za kumuongezea mkataba mpya nyota huyo mwenye makeke mengi uwanjani akiwa ametupia bao moja kwenye ligi.

Hivi karibuni, Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara aliweka wazi kwamba mchezaji huyo ana uwezo mkubwa licha ya kuwa kuna muda huwa wanatofautiana na wengine wanasema kwamba hana nidhamu.

Meneja wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ndani ya kikosi cha Simba, Ahmed Ally amesema kuwa ikiwa wanamhitaji nyota huyo wapo tayari kuwapa hata kwa mkopo.

“Wanamtaka Morrison Yanga? Ili aweze kuwapeleka hatua ya robo fainali? Sisi tupo tayari kuwapa hata kwa mkopo,”.