STRAIKA wa Real Madrid, Mohamed Salah, ameshuhudia Real Madrid ikiichapa Manchester City na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa, akafurahi na kusema: “Hawa ndio nawataka nijilipizie kisasi.”
Salah amesema anawasubiri kwa hamu Real Madrid Mei 28 jijini Paris akitaka kulipiza walivyomuumiza moyo miaka minne iliyopita, alipogongwa na Sergio Ramos akaumizwa mkono, kisha Liverpool ikapoteza fainali.
Salah, 29, aliposti kwenye Instagram juzi usiku: “Tuna suala la kuliweka sawa.”
Salah pia awali baada ya kutinga fainali Jumanne walipoitoa Villarreal alisema: “Nataka kucheza dhidi ya Madrid, ni lazima niwe mkweli.
“Manchester City ni timu imara sana, tumecheza dhidi yao mara kadhaa msimu huu. kama ukiniuliza mimi binafsi, ningependa Madrid. Tulipoteza fainali dhidi yao hapo kabla, nataka kucheza dhidi yao na natumaini tutashinda.”
‘Van Dijk ni beki bora wa wakati wote’
LIVERPOOL, England
MCHAMBUZI Michael Owen amedai beki wa Liverpool Virgil van Dijk ni beki bora wa kati wa wakati wote.
Lakini Rio Ferdinand amesema huyu ni beki bora duniani kwa sasa, siyo kwa wakati wote.
“Mimi nitaenda mbele zaidi. Nadhani ni beki bora wa kati wa wakati wote,” alisema Owen, straika wa zamani wa Liverpool.
Alipoulizwa nini kinamfanya awe bora zaidi ya Ferdinand na wengine, Owen alijibu: “Anafunga mabao pia, siyo mengi, lakini tunazungumzia ukubwa hapa.
“Kama nilivyosema, Rio alikuwa beki bora niliyewahi kucheza naye. Lakini kwa Van Dijk, kama beki mshambuliaji, namuangalia na kufikiri: unafanyaje dhidi yake?
“Ni mkubwa kuliko kila mtu, ana kasi kuliko kila mtu, ana nguvu kuliko kila mtu, ana ubora akiwa na mpira, anafunga mabao. Sijawahi kuona kitu kama hicho.
“Kitu pekee ambacho kinapwaya kwa Van Dijk kwa sasa ni medali alizoshinda. Ameshinda medali moja tu ya Premier na moja ya Ligi ya Mabingwa.
“Watu kama Rio na (Paolo) Maldini na (Franco) Baresi na watu kama hao ambao wanatajwa kuwa bora wa wakati wote, wameshinda medali nyingi.”
Van Dijk alishinda pia mataji ya ligi mara mbili mfululizo akiwa na Celtic, lakini ana kazi kubwa ya kufanya kuwafikia Sergio Ramos, Raphael Varane, Thiago Silva, Giorgio Chiellini na Vincent Kompany katika suala la medali.