YANGA WATAJA WACHEZAJI WA KUWAHOFIA SIMBA,MORRISON NDANI

MAMBO mengi yana mwisho na leo inaweza kuwa hivyo kwa kuwa watani wa jadi Yanga na Simba wanatarajiwa kumaliza zile kelele za kitaa nani mkali.

Ofisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli aliweza kufanya mahojiano maalumu na Global Radio kwenye kipindi cha Krosi Dongo aliweka wazi mipango yao namna hii:-

“Kwenye mechi za misimu mitatu tulianza kwa sare, msimu huu pia tulianza na sare na tumetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Namungo,wachezaji walipumzika siku moja kisha walianza kufanya mazoezi.

“Ni moja ya mechi ngumu,inatazamwa na wengi, muhimu ni pointi tatu ambazo Simba wanazo, sisi walipochukua ubingwa tuliwachangia na wao wanapaswa kutuchangia.

Hali za wachezaji je?

“Djuma Shaban aliumia kwenye mchezo dhidi ya Namungo ila Said Ntibanzokiza bado anaendelea na matibabu.Kuanza kwao ama kuanza itategemea mwalimu atasema nini na wataalamu watasema nini.

“Dabi ni muhimu kila mmoja analitambua, wale,(Simba) hawaeleweki wanaweza kushuka daraja ikitokea hivyo sisi tutaomba kucheza nao mchezo wa kirafiki huko watakakokuwa.

Kuna bonasi kwa wachezaji?

 “Dau lipo na wachezaji wanajua lakini hatutaweza kuliweka wazi suala hilo hata Ulaya ipo hasa masuala ya bonasi lakini kama wakiweza kushinda kuna dau kubwa hasa kwenye mechi za dabi huwa kunakuwa na utofauti.

Alama 3 za Simba zitawapa ubingwa?

 “Tukipata alama tatu itakuwa inatusogeza kwenye ule ubingwa ulipo kwa kuwa bado tunasogea kwenye ubingwa na sio tutakuwa tumechukua kwa kuwa zitakuwa zimebaki pointi kama 9 hivi.

 “Ikitokea tumefungwa haitashusha malengo yetu na sio kupoteza hata kama tungepoteza mchezo wetu tungepoteza mchezo na kusonga mbele. Sisi tukifungwa maana yake hatujapoteza malengo tumepoteza mchezo.

Unadhani Simba itachukua taji lipi?

“Simba hataweza kuchukua taji lolote kwa sasa na kwenye FA mpaka avuke hatua ya robo fainali na tabu ataipata akivuka atakuja kwetu atakutana na balaa kweli maana sisi tumetangulia.

 Mechi ipi ilikuwa na presha kubwa?

“Ile mechi ambayo tulisawazisha mbele ya Simba ya Mapinduzi Balama tulipopata sare ya kufungana mabao 2-2 kulikuwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki na sisi tunataka kuweka rekodi za kuwafunga Simba.

“Kuna ile presha huwa tunaipata, tukifungwa huwa tunapigiwa simu na viongozi wakubwa,mashabiki,kumbuka hata Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema kwamba tukifungwa huwa tunasononeka,tukishinda huwa inakuwa raha.

 

Huwa mnawafuatilia wachezaji kwa njia ipi?

“Tunawapa kila kitu ambacho wachezaji wanafanya na wanafanyiwa na hasa yale ambayo huwa yanandikwa kutoka kwenye magazeti huwa tunayafanyia kazi ikiwa ni pamoja na gazeti la Championi hawa tunajua ni wadukuzi sana kuhusu sisi yale yote huwa tunayafanyia kazi.

Kuna wachezaji wakikosekana mnapata tabu?

 “Wachezaji wote ni muhimu na tuliweza kupata sare wakiwepo wachezaji wote ikiwa ni pamoja na Feisal Salum,Khalid Aucho huwa tunakosa jambo wasipokuwepo lakini tunapata ushindi,kumbuka Azam FC tulishinda bila uwepo wa Aucho.

“Najua kwamba Saleh Ally, (Mhariri Mtendaji wa Global Group) anajua kuwa kocha mzuri huwa anaandaa plan ya game,(mpango wa mchezo) kutokana na aina ya wachezaji alionao.

Unauzungumziaje ubora wa Simba?

“Yanga inapokuwa bora inaweza kupata matokeo kwa Simba,Simba inapokuwa bora haiwezi kupata matokeo kwetu, kwa sasa licha ya kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa sio kwamba kikosi hakipo sawasawa ila walitolewa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa.

“Simba wameanza kupoteza Ngao ya Jamii, hawajaongoza ligi na hawana namna ya kuongoza ligi mpaka tutakapomaliza mzunguko hii ina maana kwamba wameweza kupungua kwenye ubora wao licha ya kuweza kufika hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho.

Wachezaji gani mnawahofia wa Simba?

“Huwezi kusema huwahofii wachezaji wa Simba itakuwa unafiki, Simba ina wachezaji wazuri, huwezi kusema haumhofii Shomari Kapombe ukamuacha Israel Mwenda.

“Clatous Chama, Morrison, (Bernard) hawa ni wachezaji wazuri.

“Simba walifanya figisu nyingi kumchukua Morrison kwa kuwa wanajua kwamba ni mchezaji mzuri na huyu ni play maker wa Simba.

“ Mayele kuelekea kwenye dabi hii aliniambia anawaheshimu mabeki wa Simba kwa kuwa wana uwezo mkubwa.

“Mayele amewataja Inonga, (Henock),Pascal Wawa,Onyango, (Joash) kwa kusema kwamba hawa wametoka nje na wana kitu, lakini hatarajii kuona wachezaji hawa wanakamia kwa kucheza michezo ya kurukiana kama ile ya Yondani, (Kelvin).

“Pamoja na purukushani zote alizopewa na Agrey Morris,(beki wa Azam FC) anasema hakutukanwa ila kwa wengine wamekuwa wakimtukana,wakimpiga mateke,viwiko ila anaamini haitakuwa hivyo kwa Simba,”amesema.